Skip to main content

Utaratibu wa amani Mali njia panda: Baraza la Usalama

Utaratibu wa amani Mali njia panda: Baraza la Usalama

Leo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limejadiliana kuhusu hali iliyopo nchini Mali na mafanikio yaliyopatikana katika kutekeleza makubaliano ya amani. Taarifa zaidi na Joshua Mmali.

(Taarifa ya Joshua)

Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa hivi karibuni ni kuundwa kwa mikoa miwili mipya kaskazini mwa nchi na kuendelea kuachia madaraka kwa serikali za mikoa.

Akihutubia Baraza hilo, mkuu wa Idara ya Ulinzi wa Amani ya Umoja wa Mataifa Hervé Ladsous amekaribisha hatua hizo, akisema hata hivyo hatua zingine za ziada zinahitajika kwa upande wa usalama, amani, na kupambana na ugaidi kwenye ukanda mzima wa Afrika magharibi.

Ameeleza umuhimu wa kuanzisha doria za pamoja kaskazini mwa nchi, ambazo zitachangia pakubwa katika utaratibu wa kujisalimisha kwa waasi na kurejesha uaminifu wa raia:

(Sauti ya Ladsous)

“Kila siku tunayopoteza katika utekelezaji wa makubaliano ya amani, ni siku ya ziada ya ushindi kwa vikundi vya ukaidi ambavyo lengo lao ni kuharibu utaratibu wa amani wa Mali, na ambavyo vinalenga wawakilishi wa serikali, wa upinzani, vikosi vya usalama vya kimataifa na vya MINUSMA.”