Skip to main content

WHO yahitaji dola bilioni 2.2 kwa masuala ya dharura

WHO yahitaji dola bilioni 2.2 kwa masuala ya dharura

Shirika la Afya Duniani WHO na wadau wa afya mwaka huu wanahitaji dola bilioni 2.2 kwa ajili ya kutoa huduma za afya za kuokoa maisha kwa watu zaidi ya milioni 79 duniani kote, mahitaji hayo ya dharura yakiwa yamefikia kiwango cha juu kabisa katika historia. Taarifa kamili na Grace Kaneiya.

(Taarifa ya Grace)

WHO imetoa ombi hilo leo ikizindua mpango wa kukabiliana na masuala ya kibinadamu ya dharura kwa mwaka 2016 ikisema kuongezeka kwa mizozo, mabadiliko ya tabianchi, ukuaji wa miji bila mipango, yote yanasababisha mahitaji ya afya ya dharura kuendelea kuongezeka.

Miongoni mwa vipaumbele vya WHO ni utoaji dawa, chanjo na vifaa tiba dhidi ya kipindupindu na surua.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi, Mkuu wa Idara ya Masuala ya dharura ya WHO Richard Brennan amesema mikakati ya dharura ya WHO ni endelevu kwani

(Sauti ya Bwana Brennan)

“Ni muhimu kujua kwamba kazi ya WHO katika masuala ya dharura inaanza kabla mzozo haujalipuka, na inaendelea muda mrefu baada ya timu ya dharura kuondoka, kwa sababu tunasaidia nchi kujitayarisha na kupona na mizozo. Na mfano mzuri ni Nepal, ambako tumefanya kazi kwa miaka mingi kuhusu mipango ya dharura pamoja na wizara ya afya, na bado tupo kule ili kusaidia sekta ya afya kukwamuka baada ya tetemeko la ardhi.”