Hatma ya Ruto na Sang ICC kujulikana saa chache zijazo
Saa chache zijazo mahakama ya kimataifa ya uhalifu, ICC huko The Hague Uholanzi itatoa uamuzi juu ya ombi la upande wa utetezi kwenye kesi dhidi ya William Ruto na Joshua arap Sang wote wa Kenya.
Upande wa utetezi uliomba kesi hiyo itupiliwe mbali kwa minajili kwamba hakuna kesi ya kujibu kwenye mashtaka dhidi ya wawili hao ambayo ni uhalifu dhidi ya ubinadamu ikiwemo mauaji, kuwafurusha watu makwao au kuwatoa watu makwao bila hiari yao na mateso.
Makosa hayo yadaiwa kufanyika mwaka wa 2007 na 2008 wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi mkuu.
Taarifa ya ICC imesema kuwa uamuzi huo utatolewa saa Kumi na Moja jioni kwa saa za The Hague, Uholanzi ambapo utatolewa kwa maandishi kwa kuwa hakutakuwepo na kikao cha mahakama.
Uamuzi huo utachapishwa kwenye tovuti ya ICC pamoja na toleo la habari litakalopelekwa kwenye vyombo mbali mbali vya habari.
Tarehe 23 Oktoba mwaka 2015 Sang alitoa ombi la kwamba hakuna kesi ya kujibu huku Ruto akiwasilisha ombi lake tarehe 26 Oktoba mwaka huo huo ya kwamba mashtaka yote yafutwe.
Majaji wanaohusika na kesi hiyo ni watatu wakiongozwa na Jaji Chile Eboe-Osuji akisaidiwa na Jaji Robert Fremr na Jaji Olga Herrera-Carbuccia.