Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuunge mkono kazi ya UNMAS- Mcheza filamu Daniel Craig

Tuunge mkono kazi ya UNMAS- Mcheza filamu Daniel Craig

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kuhusu utokomezaji wa mabomu ya kutegwa ardhini na hatari ya vilipuzi, Daniel Craig, ametoa wito leo dunia iunge mkono kazi ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloendesha shughuli za kuondoa mabomu ya kutegwa ardhini na jitihada za kibinadamu, UNMAS.

Bwana Craig amesema hayo mbele ya waandishi wa habari leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, New York, katika kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya kuelimisha kuhusu mabomu ya kutegwa ardhini na vifaa vya milipuko, leo tarehe 4 Aprili.

“UNMAS ina mchango mkubwa katika kuboresha fursa ya kunusuru maisha ya raia na wahudumu wa kibinadamu wanaonaswa katika ghasia za silaha. UNMAS hutoa suluhu ya muda mrefu kwa tatizo kubwa zaidi linalowakabili waathirika wa vita: jinsi ya kurejelea maisha ya kawaida. Nina heshima kubwa kwa watu ninaofanya nao kazi UNMAS. Nawaomba tuungane katika kupigia debe kazi yao na kufadhili programu zao ili nanyi mchangie mabadiliko.”

Naye Mkurugenzi wa huduma ya kuchukua hatua dhidi ya mabomu ya kutegwa ardhini (UNMAS), Agnès Marcaillou ameeleza zaidi kuhusu huduma ya shirika analoongoza

“UNMAS hufundisha na kutuma wataalam wa kuondoa silaha ambazo hazijalipuka, ili kuwezesha watu waliolazimika kuhama makwao na wakimbizi kurudi salama nyumbani, watoto kurejea shule - kama tulivyoona Gaza miaka michache iliyopita - kwa wakulima kupanda mimea ya chakula kwa usalama katika maeneo yaliyokuwa yamezingirwa, na kwa wahudumu wa afya kurudi katika mahospitali yaliyorushiwa mabombu.”