Wafanyakazi wa majumbani wana haki ya kupumzika- ILO
Shirika la kazi duniani, ILO limesema zaidi ya nusu ya wafanyakazi wa majumbani kote ulimwenguni bado wanakosa haki ya msingi ya binadamu ya kupumzika kutokana na kukosa ukomo wa saa za kazi siyo tu kwa siku bali kwa wiki. Flora Nducha na ripoti kamili.
(Taarifa ya Flora)
Katika kichapisho chake, ILO imesema , ukosefu wa haki hiyo ya kisheria unaweka katika kiza cha mazingira magumu ya kazi hususan wale wanaoishi na waajiri wao wakifanya kazi kwa zaidi ya saa 60 kwa wiki wengine wakiamshwa hata nyakati za usiku.
ILO inasema madhara ya kufanya kazi bila kupumzika ni pamoja na magonjwa kama vile kisukari aina ya Pili, moyo na msongo wa mawazo ambapo imesema wafanyakazi wa majumbani wanatakiwa kupumzika saa 11 kwa siku.
Philippe Marcadent mkuu wa kitengo cha mazingira ya kazi ILO amesema bado kuna mkwamo kuzingatia haki hiyo kwa kuwa kazi inafanyika majumbani licha ya kwamba mkataba wa kimataifa wa wafanyakazi wa majumbani ibara ya 189 umetaja kupumzika kama haki ya msingi.
Hata hivyo nchi kama Chile zimepongezwa kwa kuzingatia mkataba huo ikiwemo wafanyakazi wa ndani kupumzika saa 11 kwa siku huku jumamosi na jumapili wakiwa mapumziko.