Baraza kuu latangaza muongo wa lishe

Baraza kuu latangaza muongo wa lishe

Baraza kuu la Umoja wa Mataifa limetangaza leo muongo wa hatua kuhusu lishe ambao unaanza mwaka 2016 hadi 2015 ambapo shirika la kilimo na chakula FAO limepokea uamuzi huo na kusema ni hatua muhimu katika kupunguza njaa na kuimarisha lishe duniani.

Taarifa ya FAO kuhusu tangazo hilo imesema kuwa kwa kuzingatia kuwa takribani watu milioni 800 hawapati lishe bora na zaidi ya bilioni mbili wanaugua utapiamlo. Imeendelea kusema kuwa takwimu zinaonyesha watoto karibu milioni 159 walioko chini ya miaka mitano wamedumaa, milioni 50 wengine wana uzito mdogo ikilinganishwa na urefu wao huku watu bilioni 1.9 wana uzito mkubwa na milioni 600 wana utipwattipwa.

FAO imesema azimio la leo la baraza kuu limetambua umuhimu wa kuondoa njaa na kuzuia aina zote za utapiamlo duniani, pamoja na kupanua wigo kwa wadau kufanya kazi pamoja katika kutatua changamoto hizi za lishe.

Azimio hilo linalitaka shirika la chakula na kilimo FAO, shirika la afya ulimwenguni WHO kuongoza utekelezaji wa muongo wa hatua kuhusu lishe kwa kushirikiana na shirika la mpango wa chakula duniani WFP pamoja na mfuko wa maendeleo ya kilimo IFAD, na lile la Umoja wa Mataif ala kuhudumia watoto UNICEF.