Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maandalizi yanaendelea kwa ajili ya duru nyingine ya mazungumzo ya amani Yemen

Maandalizi yanaendelea kwa ajili ya duru nyingine ya mazungumzo ya amani Yemen

Maandalizi yanaendelea kwa ajili ya duru nyingine ya mazungumzo ya Yemen ambayo yatafanyika chini ya mwamvuli wa Umoja wa mataifa nchini Kuwait kuanzia Aprili 18 mwaka huu.

Mazungumzo hayo yanalengo la kufikia makubaliano ambayo yatamaliza vita na kuruhusu kuanza kwa mjadala jumuishi wa kisiasa kwa kuzingatia azimio la Baraza la Usalama namba 2216 la mwaka 2015 na maazimio mengine.

Kwa mujibu wa mwakilishi maalumu wa Umoja wa mataifa kwa ajili ya Yemen Ould Cheikh Ahmed ana matumaini ya ushiriki mzuri wa pande husika katika mazungumzo hayo na kwamba ni muhimu kwa ujumbe huo kutumia fursa hiyo kutafuta njia ya kurejesha amani na utulivu nchini mwao.

Ameongeza kuwa timu ya wataalamu wa siasa ya Umoja wa Mataifa imeshawasili sana’a na Riyadh ili kufanya kazi na wajumbe katika maandalizi ya mazungumzo hayo.

Pande zote katika vita Yemen ziliafikiana kusitisha uhasama ulioanza kutekelezwa usiku wa Aprili 10 mwaka huu.