Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban akaribisha kuwasili Tripoli kwa Baraza la Urais la Libya

Ban akaribisha kuwasili Tripoli kwa Baraza la Urais la Libya

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amekaribisha kuwasili kwa Baraza la Urais la Libya mjini Tripoli mnamo Machi 30, 2016, akitaja kuwasili huko kama hatua muhimu katika kutekeleza makubaliano ya kisiasa ya Libya.

Ban ametoa wito kwa wadau kuheshimu matamanio ya raia wengi wa Libya ya amani, ustawi na mafanikio.

Aidha, Katibu Mkuu ametoa wito kwa wadau wote na taasisi za umma zisaidie kuwezesha kukabidhi madaraka kwa njia ya amani, akikumbusha wajibu wa wale wanaosimamia usalama kuhakikisha usalama wa Baraza la Urais, na kuwahimiza wajiepushe na vitendo vyovyote vinavyoweza kuvuruga kazi ya Baraza hilo.

Ban amepongeza Baraza la Urais kwa ujasiri na uongozi wake, na kukariri u tayari wa Umoja wa Mataifa kusaidia mamlaka na watu wa Libya, ili nchi yao iendelee kwenye barabara ya mpito wa kidemokrasia.