Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama laziomba nchi za Maziwa Makuu kutimiza ahadi zao

Baraza la Usalama laziomba nchi za Maziwa Makuu kutimiza ahadi zao

Wanachama wa Baraza la Usalama leo wamekuwa na mjadala maalum kuhusu Mchakato wa amani,usalama na ushirikiano kwa ajili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na ukanda wake, wakizisihi nchi wanachama kutimiza ahadi zao ili kupata amani ya kudumu.

Taarifa iliyotolewa leo na Rais wa Baraza hilo imeelezea pia wasiwasi wa wanachama hao kuhusu michakato ya uchaguzi kwenye baadhi ya nchi za ukanda wa maziwa makuu, ikisema kwamba inaweza kusababisha vurugu na ghasia kwenye ukanda mzima.

Aidha wanachama hao wamesisitiza umuhimu wa kujisalimisha kwa waasi wa FDLR, LRA, ADF na Mai-Mai na kuimarishwa kwa ushirikiano kati ya jeshi la kitaifa la DRC FARDC na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo MONUSCO.

Wamezihimiza pia serikali za ukanda huo kutowapa hifadhi watekelezaji wa uhalifu wa kivita na kutosaidia vikundi vilivyojihami, pamoja na kuwajibisha waliotekeleza vitendo vya ukikwaji wa haki za binadamu.

Halikadhalika, wamemulika tatizo la biashara haramu ya mali asili, wakisema hiyo pia ni moja ya vyanzo vya mzozo unaoathiri Mashariki mwa DRC.

Miongoni mwa suluhu zinazopendekezwa na taarifa hiyo ni uwekezaji zaidi katika ajira ya vijana, usawa wa jinsia, biashara halali ya mali asili na ushirikiano wa kikanda.