Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lapitisha azimio la kudhibiti uuzaji wa mafuta na silaha Libya

Baraza la Usalama lapitisha azimio la kudhibiti uuzaji wa mafuta na silaha Libya

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, leo limepitisha azimio la kuongeza muda wa mamlaka ya vikwazo vilivyowekewa Libya chini ya azimio lake namba 2146 la mwaka 2014, hadi Julai 31 mwaka 2017.

Baraza la Usalama pia limelaani majaribio ya uuzaji haramu wa mafuta ghafi ya Libya nje, ukiwemo ule unaofanywa na taasisi ambazo hazipo chini ya mamlaka ya serikali ya makubaliano ya kitaifa (GNA).

Aidha, Baraza limetoa wito kwa serikali ya makubaliano ya kitaifa iteue mtu atakayekuwa akiwasiliana na kamati iliyowekwa na azimio lake namba 1970 (2011), kuhusu utekelezaji wa hatua zilizoagizwa na azimio 2146 (2014), na kuifahamisha kamati hiyo kuhusu vyombo vya usafiri vinavyosafirisha mafuta ghafi ya Libya kiharamu.

Azimio hilo pia limeitaka serikali ya Libya kutoa taarifa za mara kwa mara kuhusu bandari, visima vya mafuta na majengo yaliyo chini ya mamlaka yake, na kuhusu njia zinazotumiwa kuhakiki uuzaji halali wa mafuta ghafi nje, pamoja na uagizaji na uuzaji wa silaha.

Aidha, azimio hilo limeitaka serikali ya makubaliano ya kitaifa iteue mtu atakayetoa taarifa kwa kamati hiyo kuhusu mfumo wa vikosi vya usalama vilivyo chini ya serikali, miundombinu iliyopo ya kuhakikisha hifadhi, usajili, utunzaji na usambazaji salama wa vifaa vya kijeshi na mahitaji ya mafunzo, pamoja na kusisitiza umuhimu wa serikali hiyo kuwa na udhibiti bora wa hifadhi salama ya silaha, kwa usaidizi wa jamii ya kimataifa.