Kamishna wa haki za binadamu asikitishwa na ripoti mpya ya ukatili wa kingono CAR

Kamishna wa haki za binadamu asikitishwa na ripoti mpya ya ukatili wa kingono CAR

Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu Zeid Ra’ad Al Hussein ameelezea huzuni yake kuhusu ripoti mpya za ukatili wa kingono uliofanywa na walinda amani wa Umoja wa Mataifa na Ufaransa kwenye eneo la Kemo nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR, kati ya mwaka 2013 na 2015.

Kwenye taarifa iliyotolewa leo, Bwana Zeid amesema tayari uchunguzi wa dhati unafanyika, na nchi tatu husika zimeshajulishwa, Zeid akizisihi nchi hizo kuchukua hatua zaidi. Pamoja na askari wa ujumbe wa Ufaransa Sangaris, vikosi vya walinda amani kutoka Gabon na Burundi wanashukiwa kutekeleza uhalifu huo.

Kwa upande wake msemaji wa Umoja wa MAtaifa Stéphane Dujarric amesema vikosi vya Burundi na Gabon wamelazimishwa kubaki ndani ya kambi ya MINUSCA hadi uchunguzi umalizike, huku wanachama wa Baraza la Usalama wakitakiwa kujadili suala hilo leo kwenye mkutano wa faragha.

Aidha akizungumza na waandishi wa habari, Bwana Dujarric ameongeza kwamba Mfuko wa Msaada kwa wahanga wa ukatili huo utaanzishwa hivi karibuni.

(Sauti ya Dujarric)

“Fedha zitatumiwa kutoa huduma za kiafya, kisheria, na kisaikolojia kwa wahanga wa ukatili wa kingono na watoto waliozaliwa kutokana na ubakaji huo.”