Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nuru yaonekana CAR katika utaratibu wa mpito

Nuru yaonekana CAR katika utaratibu wa mpito

Awamu ya pili ya uchaguzi wa wabunge inafanyika leo nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR, siku moja tu baada ya kuapishwa kwa rais mteule Faustin Archange Touadera jumatano hii, kwenye uwanja wa mpira wa mji mkuu Bangui.

Katika hotuba yake, Rais Touadera amezingatia masuala anayotaka kuyawekea kipaumbele, yakiwa ni usalama wa taifa, kujisalimisha kwa waasi, kuimarisha jeshi na kupambana na ufisadi.

Akihojiwa na Radio ya Umoja wa Mataifa Guira FM baada ya hafla hiyo, mkuu wa idara ya operesheni za ulinzi wa amani ya Umoja wa Mataifa Hervé Ladsous, ameelezea matumaini yake

(Sauti ya Ladsous)

“Tukikumbuka hali iliyokuwepo nchini humo miaka miwili au mitatu iliyopita, tunaona kabisa kwamba mafanikio yamepatikana. Inatia moyo. Nani angeweza kutumaini hivyo miaka mitatu iliyopita? Ni hatua muhimu sana. Sasa ni lazima kuendelea na bidii nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati ili kudumisha maendeleo na maridhiano.”