Skip to main content

Kutokuwepo usawa katika masuala ya afya mijini ni changamoto:WHO/UN-HABITAT

Kutokuwepo usawa katika masuala ya afya mijini ni changamoto:WHO/UN-HABITAT

Takwimu mpya kuhusu afya ya wakazi wa mijini kutoka takribani nchi 100 zinaonyesha kwamba, wakati idadi ya wakazi wa mijini ikiongezeka, kutokuwepo kwa usawa katika masuala ya afya hususani baina ya matajiri na maskini ni changamoto inayoendelea. Hii ni kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa kwa pamoja na shirika la afya duniani WHO na shirika la Umoja wa Mataifa la makazi UN-Habitat.

Mashirika hayo yamesema nusu tu ya nyumba katika mataifa 91 mijini ndio zina fursa ya kupata maji ya bomba huku matajiri ambao ni asilimia 20 wana fursa hiyo mara 2.7 ikilinganishwa na maskini. Kwa Afrika uwiano ni karibu mara 17 zaidi. Ripoti inasema watu wapatao bilioni 3.7 wanaishi mijini hivi leo na wengine bilioni 1 wataongezeka ifikapo 2030, na ni ongezeko la asilimia 90 kwa nchi za kipato cha chini na wastani.

Imeongeza kuwa hali hii inatoa msisitizo wa kuhakikisha malengo ya maendeleo endelevu SDG’s yanafikiwa na hasa katika kuhakikisha huduma ya afya kwa wote, na kwamba watu wote wanaopatiwa huduma za afya wanahitaji kumudu bila gharama kubwa ifikapo 2030.

Pia ripoti imebaini kwamba katika nchi 79 za kipato cha chini na wastani watoto masikini mmoja kati ya watano wanauwezekano wa kufa kablya ya kutimiza miaka mitano ikilinganishwa na watoto katika mataifa tajiri. Na imesisitiza uharaka wa kushughulikia pengo lilililopo katika masuala ya afya na vyanzo vyake mijini hasa wakati mataifa yakijitahidi kufikia malengo ya SDG’s na kubaini njia za kuyaziba mapengo hayo.