Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa MINUSCA akariri msimamo wake dhidi ya ukatili wa kingono

Mkuu wa MINUSCA akariri msimamo wake dhidi ya ukatili wa kingono

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR, Parfait Onanga-Anyanga, amelezea dhiki yake kuhusu vitendo vya ukatili wa kingono vilivyoripotiwa kufanyika na walinda amani wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa anaoongoza nchini humo, MINUSCA.

Kwenye makala aliyoandika katika gazeti la Newsweek, Bwana Onanga-Anyanga ameeleza kwamba siku chache zilizopita alipokea taarifa ya kesi nyingine ya ubakaji dhidi ya msichana mwenye umri wa miaka 14, ambayo inafuatia ripoti za vitendo vingine kadhaa vilivyoripotiwa kufanyika mwaka 2014 na 2015.

Mkuu huyo wa MINUSCA amekariri utashi wake wa kusitisha vitendo hivyo kupitia mkakati wa uwazi na uwajibikaji. Amesema tayari MINUSCA imeandaa timu maalum ya kufuatilia kesi hizo na tabia za walinda amani kwa ujumla, pamoja na kutoa msaada wa dharura kwa wahanga wa ukatili wa kingono.

Aidha, ameongeza kwamba kupitia azimio 2272 la Baraza la Usalama, Umoja wa Mataifa umeamua kwamba, iwapo serikali za nchi husika hazitachukua hatua dhidi ya askari waliotekeleza uhalifu wa aina hiyo katika kipindi cha miezi sita, basi Katibu Mkuu Ban Ki-moon ataruhusiwa kuondoa kikosi kizima, jinsi alivyofanya dhidi ya walinda amani wa Congo na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC nchini CAR.