Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtalaam wa UM apata hasira kuhusu mauaji ya mpalestina Hebron

Mtalaam wa UM apata hasira kuhusu mauaji ya mpalestina Hebron

Video ya raia wa Palestina aliyeuawa na askari wa Israel akiwa amejeruhiwa na kulala chini imemtia hasira mratibu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu mauaji ya kiholela Christof Heyns.

Hii ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo kufuatia mauaji yaliyofanyika wili iliyopita mjini Hebron, kwenye ukingo wa magharibi, yakiripotiwa na shirika la haki za binadamu la Israel ambalo lilitoa video hiyo. Ripoti inaeleza kwamba mpalestina huyo amepigwa risasi baada ya kumchoma kisu askari wa Israel.

Bwana Heyns amesema video hiyo inaonyesha kitendo kinachoonkena kabisa kuwa mauaji ya kiholela, akiongeza kwamba ni uhalifu kuua mtu ambaye tayari amedhibitiwa na siyo hatari tena kwa wengine.

Juu ya hayo, ameelezea wasiwasi wake kuhusu jinsi askari wengine na madaktari ambavyo hawakumjali hata kidogo raia huyo, wakiwa wanamhudumia askari wa Israel pekee ambaye alikuwa na majeraha madogo.

Hata hivyo Bwana Heyns amekaribisha ripoti ya kukamatwa kwa askari huyo, akisisitiza umuhimu wa kuendeleza uwajibikaji kwa pande zote, na kuongeza kwamba jumla la wapalestina 133 na waisraeli 30 wameuawa tangu mwanzo wa mivutano ya hivi karibuni mwezi October.