Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

MONUSCO yaongezwa mwaka mmoja DRC

MONUSCO yaongezwa mwaka mmoja DRC

Baraza la Usalama leo limepitisha azimio la kuongeza muda wa mamlaka ya Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC MONUSCO kwa mwaka mmoja hadi Machi, 31, 2017, pia likiamua kutopunguza zaidi idadi ya walinda amani, hadi hali ya usalama itakapoimarika.

Azimio lililopitishwa leo limeelezea wasiwasi wa wanachama wa Baraza hilo kuhusu kuzidi kuzorota kwa hali ya usalama na ya kibinadamu mashariki mwa nchi kufuatia mapigano ya waasi na mivutano ya kikabila, likisisitiza umuhimu wa kujisalimisha vikundi vya waasi vya FDLR, ADF, LRA na vingine, na kurejeshwa kikamilifu kwa ushirikiano kati ya MONUSCO na jeshi la kitaifa FARDC.

Aidha azimio hiyo limeiomba serikali ya DRC kuhakikishia utaribu wa wazi na jumuishi wa uchaguzi, likielezea wasiwasi mkubwa kuhusu kuchelewa kwa ratiba ya uchaguzi unaotarajia kufanyika mwisho wa mwaka huu, na ripoti za ukiukwaji wa haki za binadamu unaoripotiwa kutekelezwa na askari wa polisi.

Wanachama wa Baraza hilo wameiomba serikali ya DRC iongeze bidii katika kuimarisha utawala wa sheria, maridhiano na demokrasia ili kudumisha amani na usalama nchini humo.