Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Japan yaitolea msaada UNICEF kusaidia watoto Burundi

Japan yaitolea msaada UNICEF kusaidia watoto Burundi

Japan imelitolea shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), msaada wa Dola Milionioni moja na laki tatu za Kimarekani kusaidia watoto nchini Burundi. Msaada huo utasaidia hasa kupambana na maradhi ya utapia mlo katika mikoa mitano ya Burundi, wakati takwimu zikionyesha kuwa nusu ya watoto chini ya umri wa miaka mitano nchini humo wanasumbuliwa na tatizo la utapiamlo.

Kutoka Bujumbura, Mwandishi wetu Ramadhani KIBUGA anasimulia zaidi

(Taarifa ya Kibuga)

Msaada huo wa Japan utalisaidia Shirika la UNICEF Burundi na washirika wake kutoa msaada kwa watoto wenye matatizo. Pia msaada huo utawezesha kuwapa huduma watoto Elfu 10 wanaosumbuliwa na tatizo kubwa la utapiamlo katika mikoa ya Cankuzo, Kirundo, Makamba, Rutana na Ruyigi, na kuwasaidia watoto na wakaazi zaidi ya laki moja kupata maji safi katika tarafa ya Nyanzalac, mkoani Makamba.

Mwakilishi wa UNICEF Burundi Bo Vikhor Nylund amesema msaada huo umekuja wakati muafaka kwa watoto wa Burundi, kwani inadhihirika kuwa idadi ya watoto wenye matatizo inazidi kuongezeka, na hivyo uwekezaji wa kuendelea ni muhimu ili kuwasaidia watoto hao.

Naye balozi mdogo wa Japan nchini Burundi anayekaa mjini Kigali, Tomio Sakamoto, amesema Japan inatilia maanani saana maisha na afya ya watoto, na ndio maana ikaamua kusaidia wakati huu ambapo msaada huo ukihitajika zaidi.

Taakwimu zinaonyesha kuwa sababu kubwa ya vifo vya watoto wa chini ya miaka mitano nchini Burundi ni maradhi ya kupumua, kuharisha na maleria. Maradhi hayo yanazidishwa na tatizo la utapia mlo, ambao unagusa zaidi ya nusu ya watoto wenye umri chini ya miaka mitano katika nchi nzima.

Shirika la UNICEF linakadiria kuwa katika mwaka wa 2016, watoto Elfu 50 wa chini ya umri wa miaka mitano wanasumbuliwa na utapia mlo kwa kiwango kikubwa, na wamekuwa na shida ya kupata msaada unaofaa. Kwa maana hiyo, limesema shirika la UNICEF, msaada wa Japan wa Milioni 1.33 za dola utashughulikia sehemu ya kero ya watoto.