Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wasiwasi wa MONUSCO kuhusu kufungwa kwa kambi ya wakimbizi ya Mpati DRC

Wasiwasi wa MONUSCO kuhusu kufungwa kwa kambi ya wakimbizi ya Mpati DRC

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC MONUSCO umeeleza leo kuziomba mamlaka za serikali ya jimbo la Kivu Kaskazini kuangazia upya uamuzi wao wa kufunga kambi ya wakimbizi wa ndani ya Mpati, inayowapa hifadhi watu wapatao 20,000.

Uamuzi huo umetangazwa na serikali ya jimbo kufuatia machafuko yaliyotokea siku chache zilizopita baina ya jeshi la kitaifa FARDC na kundi la waasi wa FDLR ambapo askari kadhaa wa FARDC wameuawa ndani ya kambi, akiwemo nahodha mmoja.

Kupitia akaunti yake ya Twitter MONUSCO imesema kufunga kambi ya Mpati ni uamuzi huru wa mamlaka za serikali, ikiongeza kwamba MONUSCO na mashirika ya kibinadamu yatatuma ujumbe wa kutathmini hali ya kibinadamu kwenye eneo hilo na kupelekea misaada wakimbizi wa ndani wa kambi hiyo haraka iwezekanavyo.

Kwa mujibu wa radio Okapi, wakimbizi wote 20,000 wa kambi hiyo wamekimbia kufuatia machafuko hayo na kutafuta hifadhi kwenye vijiji jirani.