Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kutokuwepo usawa wa kiuchumi kumeongezeka maradufu: ECOSOC

Kutokuwepo usawa wa kiuchumi kumeongezeka maradufu: ECOSOC

Pengo la kutokuwepo kwa usawa wa kiuchumi limekuwa likiongezeka duniani kwa mujibu wa Oh Joon,  Rais wa baraza la kiuchumi na kijamii kwenye Umoja wa Mataifa ECOSOC.

Akizungumza kwenye mkutano maalumu kuhusu kutokuwepo usawa mjini New York hii leo amesema watu 7 kati ya 10 duniani wanaishi kwenye nchi ambazo kukosekana kwa usawa kumeongezeka kwa kiwango cha juu sana kushuhudiwa katika miaka 30, huku asilimia moja ya matajari wakimiliki kila kitu. Na ameongeza kuwa kutokuwepo usawa ni suala lenye wigo mpana.

(Sauti ya Bwana Oh Joon)

"Kutokuwepo usawa ni zaidi ya tofauti za kipato na utajiri. Kumezungukwa na kutokuwepo fursa sawa ya upatikanaji wa mahitaji ya msingi ya binadamu kama chakula, huduma za afya, elimu, maji ya kunywa, na usafi wa mazingira." 

Amesema mkutano huu muhimu umekuja wakati ambapo awamu ya kwanza ya utekelezaji wa ajenda ya maendeleo endelevu ya 2030 imeanza na ni muhimu kuhakikisha pengo la kutokuwepo usawa linazibwa ili kufikia malengo hayo.