Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ni lazima tugawane majukumu ya kuwasaidia wakimbizi wa Syria- Ban

Ni lazima tugawane majukumu ya kuwasaidia wakimbizi wa Syria- Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amesema mzozo wa wakimbizi wa Syria, ambao ndio mkubwa zaidi kwa nyakati hizi, unahitaji usaidizi wa aina yake kutoka kwa nchi wanachama, na kuimarisha kwa mshikamano wa kimataifa kwa kiwango kikubwa. Taarifa kamili na Flora Nducha

(Taarifa ya Flora)

Ban amesema hayo kwenye mkutano wa ngazi ya juu kuhusu wajibu wa kimataifa wa kugawana majukumu ya kuwasaidia wakimbizi wa Syria.

Akizungumza kuhusu haja ya kufanya kila liwezekanalo kuwasaidia wakimbizi wa Syria, Ban amesema miaka mitano tangu kuanza mzozo huo, Wasyria wanapoteza matumaini ya kuweza tena kukidhi mahitaji ya familia zao au kuwaelimisha watoto wao.

“Watu wengi wanathamini matumaini hayo zaidi kuliko maisha yao binafsi, kama tulivyoona kwenye pwani ya Uturuki na Ulaya kusini. Jamii zinazowapa hifadhi wakimbizi katika nchi jirani zimefilisika. Afya, elimu na miundombinu ya umma imebanwa na kupungukiwa kwa rasilmali.”

Akigusia utaratibu mpya uliozinduliwa katika kongamano la London la mwezi Februari mwaka huu kuhusu kuisaidia Syria na ukanda mzima, Ban amekariri kanuni tatu za utaratibu huo

“Mosi, ni lazima tuwape wakimbizi wa Syria matumaini ya mustakhbali bora, na vifaa vya kujenga maisha yao wenyewe. Pili, ni lazima tutoe usaidizi mkubwa zaidi kifedha na kisiasa kwa jamii zinazowapa hifadhi, ili ziwe imara zaidi, na thabiti zaidi. Na tatu, ni lazima tugawane majukumu, ikiwemo kwa kupanua njia za kisheria za wakimbizi kuingia nchi nyingi zaidi”