Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maisha ya wakimbizi wa Mali nchini Burkina Faso hatarini

Maisha ya wakimbizi wa Mali nchini Burkina Faso hatarini

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula WFP na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuhudumia Wakimbizi UNHCR zimeonya kwamba maisha ya wakimbizi wa Mali 31,000 waliotafuta hifadhi nchini Burkina Faso yatakuwa hatarini iwapo hawataendelea kupewa msaada wa kibinadamu wa dharura.

Mkuu wa WFP nchini Burkina Faso ameeleza kwenye taarifa iliyotolewa leo kwamba wengi wa wakimbizi wanaoishi kambini wanategemea misaada ya kibinadamu tu kwa chakula na mahitaji yao ya msingi, akitegemea hali kuzorota zaidi wakati msimu wa mwambo ukikaribia.

Mwaka 2015, WFP imesaidia wakimbizi 31,000 kupitia msaada wa vifurushi vya chakula na fedha, ambao ilipaswa kuusitisha mwisho wa mwaka uliopita kutokana na ukosefu wa ufadhili. Mwaka huu, imebidi WFP ipunguze kiasi cha chakula kinachotolewa kwa kila mtu.

WFP imesema inahitaji dola milioni 2.5 kwa mwaka 2016, ikiwa haitegemei wakimbizi hao kurudi makwao kaskazini mwa Mali ambapo bado hali ya usalama haijaimarika.