Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vijana wana jukumu kubwa katika vita dhidi ya ukimwi: Ndaba na Kweku Mandela

Vijana wana jukumu kubwa katika vita dhidi ya ukimwi: Ndaba na Kweku Mandela

Wajukuu wa Hayati Nelson Mandela aliyekuwa Rais wa zamani wa Afrika Kusini na mwanaharakati wa kimataifa wa haki za binadamu, wamesema mchango wa vijana ni muhimu sana katika vita dhidi ya ukimwi.

Kweku Mandela na Ndaba Mandela wakizungumza kwenye kongamano la ukimwi mjini Moscow, Urusi wamesema wanaamini kazi wanayofanya ya kushiki kampeni ya vita dhidi ya ukimwi inasaidia hasa kuondokana na unyanyapaa na pia kuelimisha jamii kuona HIV na ukimwi ni kama maradhi mengine yanayohitaji mshikamano kuyakabili.

Ndaba ambaye alipoteza wazazi wake wote kwa maradhi ya ukimwi ni mwanaharakati dhidi ya ukimwi..

(SAUTI YA NDABA)

“Imekuwa ni kitu kizuri kupambana na HIV na ukimwi, hususani kutoa taarifa ya jinsi gani watu waende kupimwa, jinsi gani watu wanaweza kujilinda, na jinsi gani watu wanaweza kuelimisha jamii zao kuhusu tatizo hili muhimu”

Naye Kweku Mandela mtayarishaji mashuhuri wa filamu na msemaji wa kimataifa wa kampeni ya “Linda Lango” au UNAIDS anasema mafanikio makubwa ya kupambana na ukimwi Afrika ya Kusini yametokana na vuguvugu la vijana

(SAUTI YA KWEKU)

Mafanikio mengi yamechagizwa na wanaharakati vijana ambao kwa muda mrefu kwa sababu serikali ilikataa kutoa dawa na kutambua ukubwa wa tatizo la HIV na ukimwi ilibidi wachukue msimamo na kupigia upatu dawa bora na za bei nafuu, na kwa sababu hiyo waliweza kupatiwa dawa na kuanzisha vuguvugu la kimataifa ambapo raida wanashinikiza serikali zao”