Kupambana na njaa na kuongeza kipato vijijini kunaweza kuleta amani:FAO

29 Machi 2016

Kuimarisha uhakika wa chakula kunaweza kusaidia kujenga amani endelevu na hata kuzuia kufurukuta kwa migogoro amesema mkurugenzi mkuu wa shirika la chakula na kilimo FAO, José Graziano da Silva, akiwahutubia wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York.

Bwana da Silva amesema inatambulika kuwa hatua za kuchagiza usalama wa chakula kusaidia kuzuia migogoro, kupunguza athari zake na kusaidia ujenzi mpya na kupoza machungu baada ya vita.

Amesema machafuko ni chachu kubwa ya migogoro ya muda mrefu, ambapo uwezekano wa njaa huwa mara tatu zaidi ya sehemu zingine zinazoendelea duniani, huku nchi zenye kiwango kikubwa cha kutokuwa na uhakika wa chakula mara nyingi huwa ndizo zilizoathirika na vita akitolea mfano migogoro ya Syria, Yemen, Sudan Kusini, Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) na Somalia.

Akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha usalama wa chakula Graziano amesema katika kufanikisha ajenda ya maendeleo endelevu ya 2030 lazima kuhakikisha usalama wa chakula, kwani ameongeza kuwa hakutakuwa na maendeleo endelevu bila amani, na hakuna amani bila maendeleo endelevu.

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter