Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukosefu wa ajira ni hatari kwa Afrika Kaskazini: Ban

Ukosefu wa ajira ni hatari kwa Afrika Kaskazini: Ban

Ukosefu wa ajira, hasa kwa vijana ni changamoto kubwa inayokumba nchi zinazoendelea hasa Afrika Kaskazini, amesema leo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon akihutubia Kongamano la Kitaifa kuhusu ajira, mjini Tunis, nchini Tunisia. Taarifa kamili na Priscilla Lecomte.

(Taarifa ya Priscilla)

Bwana Ban ameeleza kwamba asilimia 30 ya vijana kwenye ukanda huo wamekosa ajira, wakiwa hatarini ya kushawishiwa na vikundi venye itikadi kali na katili.

Katibu Mkuu amesisitiza kwamba kuzalisha ajira zenye utu ni kipaumbele cha Umoja wa Mataifa, kupitia ajenda ya maendeleo endelevu.

Amemulika hatua zinazoweza kuchukuliwa na Tunisia ili kupunguza idadi ya vijana wanaokosa ajira baada ya kutimiza masomo ya ngazi ya juu, zikiwa ni pamoja na kuwekeza katika sekta mpya za uchumi, kupunguza urasimu, kuwezesha wanawake na kujenga ubia na sekta binafsi.

Hatimaye, akiwahimiza vijana wa Tunisia kuchangia katika kujenga mustakhabali bora, akisema anamini kwamba wengiwanashiriki kwenye shughuli za kijamii, au miradi ya mamlaka za serikali. Ameongeza kwamba anategemea utashi wa vijana, uwezo wao wa kushikamana na ubunifu wao ili kuleta mabadiliko na kuchangia katika maendeleo endelevu ya Tunisia.