Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Usalama mdogo wa chakula wachangia watu kukimbia Sudan Kusini:UNHCR

Usalama mdogo wa chakula wachangia watu kukimbia Sudan Kusini:UNHCR

Shirika la Umoja wa mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limesema linatiwa hofu na ongezeko la watu wanaokimbia kutoka Sudan Kusini kuingia Sudan kwa sababu ya usalama mdogo wa chakula uliosababishwa na vita vinavyoendelea na kuzorota kwa hali ya kiuchumi.

Limesema hali hiyo imesababisha watu 38,000 hasa wa maeneo ya Kaskazini mwa Bahr El Ghazal na Warrap, kukimbilia Dafur Mashariki na Kusini nchini Sudan tangu mwezi Januari.

UNHCR inahofia hali inaweza kuwa mbaya zaidi haraka kutokana na lishe duni inayoendelea kushika kasi hasa jimbo la Upper Nile, eneo la Warrap, na Kaskazini mwa Bahr Ghazal kama anavyofafanua msemaji wa UNHCR Adrian Edward

(Sauti ya Adrian Edwards)

“Watu wengi waliowasili kwenye eneo la Kordofan Magharibi, Darfur Kusini na Mashiriki wamewasili kwenye hali mbaya kabisa. Ujumbe wa pamoja wa mashirika ya kibinadamu unatathmini mahitaji sasa hivi lakini tayari ni wazi kwamba matatizo ni mengi. Watu wamekosa chakula njiani, na wanahitaji msaada wa dharura wa msingi.”