Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto Yemen wako njia panda wakati taifa likiwa hatarini kushindwa:UNICEF

Watoto Yemen wako njia panda wakati taifa likiwa hatarini kushindwa:UNICEF

Vita na kuendelea kuzorota haraka kwa hali ya kibinadamu kumeathiri maisha ya mamilioni ya watoto nchini Yemen na kulifikisha taifa hilo katika hatari ya kusambaratika. Hii ni kwa mujibu wa ripoti ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF iitwayo "watoto hatarini” inayopainisha mzigo mkubwa wa vita hivyo wanaoubeba watoto nchini yemen na kuzotora kwa hali ambayo tayari ilikuwa mbaya. Grace Kaneiya na taarifa zaidi

(TAARIFA YA GRACE)

UNICEF inathibitisha vitendo zaidi ya 1560 vya ukiukwaji wa haki za watoto, vilivyosababisha 900 kuuawa na wengine zaidi ya 1300 kujeruhiwa kwa mwaka uliopita pekee, na kwa wastani wa watoto sita kufa au kujeruhiwa kila siku kwa mujibu wa afisa wa UNICEF Julien Harneis akizungumza kutoka Sana'a

(SAUTI YA JULIEN HARNEIS)

"Kinachoendelea kila siku ni hali ya kutisha kwa watoto nchi  nzima na athari zake, mjini Taizz kuna mzunguko wa mapigano ambao unawafanya watoto kuwa katikati ya vita, wakiuawa na walenga shabaha, au makombora, maroketi na mizinga , mapigano ambayo yameshika kasi mjini Taizz"

UNICEF inasema idadi ya mwaka jana ni mara saba ya ilivyokuwa 2014 na watoto wanalipa gharama kubwa ya vita ambavyo hawakuvianzisha, ikithibitisha visa 848 vya watoto kuingizwa katika jeshi kushiriki vita na pande zote za mgogoro wengine wakiwa na umri wa miaka 10 tu.