Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwaka mmoja wa mzozo Yemen, hali ya afya yazidi kuzorota

Mwaka mmoja wa mzozo Yemen, hali ya afya yazidi kuzorota

Wakati mzozo unaoikumba Yemen ukitimiza mwaka mmoja wiki hii, Shirika la Afya Duniani WHO limeonya kwamba mamilioni ya raia wanahitaji huduma za afya nchini humo, huku asilimia 25 ya vituo vya afya vikiwa vimefungwa kwa sababu ya kubomolewa na makombora, madaktari kuuawa au kukimbia.

Kwenye taarifa iliyotolewa leo, WHO imeeleza kwamba Wayemeni milioni 14 wanahitaji huduma za afya za dharura, wakiwemo watoto milioni mbili walioathirika na utapiamlo na wanawake wanaonyonyesha.

Halikadhalika WHO imesema watu wapatao milioni 19 wamekosa huduma za maji safi na salama wakiwa katika hatari ya kuambukizwa malaria, kipindupindu na homa ya dengue.

WHO imeeleza kwamba imefanikiwa kusambaza tani 450 za vifaa vya tiba, ikiwa kupitia usafiri wa boti na punda katika sehemu zisizofikika kwa barababara.

Kwa ujumla, watu zaidi ya 6,200 wameuawa na wengine 30,000 kujeruhiwa tangu mwanzo wa mzozo mwaka mmoja uliopita.