Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban aomboleza kifo cha msichana Raquelina Langa wa Musumbiji

Ban aomboleza kifo cha msichana Raquelina Langa wa Musumbiji

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, ameeleza kupokea kwa huzuni mkubwa habari za kifo cha msichana Raquelina Langa kutoka Musumbiji, ambaye alipata umaarufu wa kimataifa alipokuja kuwa mgeni wake mashuhuri kwenye Siku ya Kimataifa ya Vijana mnamo Agosti 12, 2014.

Bwana Ban alikutana na Raquelina kwanza mnamo mwaka 2013, alipoitembelea shule ya msichana huyo mjini Maputo. Wakati huo, Raquelina alimuuliza Katibu Mkuu iwapo msichana kama yeye angeweza kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, na nini alichopaswa kufanya ili aifikie ndoto hiyo.

Katika kumpa jawabu, na pia ili kumhamasisha, Bwana Ban alimwalika Raquelina kuja kwenye Umoja wa Mataifa jijini New York, ili ajionee mwenyewe ilivyo kuwa Katibu Mkuu kwa siku moja.

Akiwasilisha ujumbe wake mbele ya waandishi wa habari leo jijini New York, Msemaji wa Katibu Mkuu, Stephane Dujarric amesema

“Katika barua kwa familia yake, Katibu Mkuu ametuma ujumbe wa rambirambi kufuatia kifo chake. Amesema ingawa maisha yake yamekuwa mafupi, sifa yake itabaki kwa muda mrefu. Raquelina alikuwa zaidi ya mtu mwenye akili kwa Musumbiji. Alikuwa mfano wa kwa nini ulimwengu unapaswa kuwekeza katika afya, maslahi, na mustakhbali wa wasichana kila mahali.”