Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lajadili wanawake, amani na usalama

Baraza la Usalama lajadili wanawake, amani na usalama

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, limekuwa na mjadala wa wazi kuhusu wanawake, amani na usalama, likimulika hasa mchango wa wanawake katika kuzuia na kutanzua mizozo barani Afrika. Taarifa kamini na Amina Hassan.

(Taarifa ya Amina)

Mjadala huo umehutubiwa na maafisa wa ngazi ya juu katika Umoja wa Mataifa, akiwemo Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika linalohusika na masuala ya wanawake, UN Women, Phumzile Mlambo-Ngcuka.

Bi Mlambo-Ngcuka amesema mchango wa wanawake katika kuzuia mizozo unaendelea kutambuliwa, ingawa mara nyingi haidhihiriki katika mazungumzo kuhusu amani na usalama katika ngazi ya juu.

Mkuu huyo wa UN Women amesema utafiti wa kimataifa wa mwaka 2015 kuhusu wanawake, amani na usalama, ulionyesha kuwa nchi zilizoendeleza usawa wa jinsia hujiepusha na matumizi ya nguvu, na kwamba usalama wa wanawake ni ishara nzuri ya amani ya nchi.

“Wanawake huwa wa kwanza kugundua kubinywa kwa haki na uhuru wao, na pale watu katika familia na jamii zao wanapoingizwa jeshini au kuandama itikadi kali. Wana ugunduzi na maarifa muhimu, ambayo pia ni muhimu katika kufanya uamuzi. Kufanyia marekebisho na kuimarisha kazi ya Umoja wa Mataifa ya kuzuia, ni lazima kujuishe mashauriano ya mara kwa mara ya Baraza hili, yanayotokana na mitazamo na tathmini za wanawake mashinani."