Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sudan yasaini mkakati wa kulinda watoto vitani

Sudan yasaini mkakati wa kulinda watoto vitani

Katika hatua muhimu ya kulinda watoto nchini Sudan, serikali ya nchi hiyo imetia saini mpango mpya wa kuchukua hatua, ili kuzuia vikosi vya usalama vya serikali kusajili na kutumikisha watoto vitani.

Umoja wa Mataifa umekaribisha dhamira hiyo ya serikali ya Sudan ya kuwalinda watoto dhidi ya ukiukwaji wa haki zao na unyanyasaji katika vita vya silaha.

Kufuatia kutiwa saini mkakati huo kwa pamoja na Umoja wa Mataifa, Waziri wa Maslahi ya Kijamii nchini Sudan, Ibrahim Adam Ibrahim, amesema serikali yake itafanya kazi kulinda haki za watoto katika mazingira ya vita vya silaha na walikolazimika kuhama makwao, pamoja na kuimarisha sera zilizopo, ambazo zimejumuishwa katika sheria kuhusu mtoto ya mwaka 2010, na sheria ya vikosi vya jeshi.

Wenyekiti wenza wa kikosi kazi cha Umoja wa Mataifa nchini Sudan, wakiwa ni Naibu Mwakilishi maalum wa Muungano wa Afrika na Umoja wa Mataifa, Bintou Keita, Mratibu Mkaazi wa masuala ya kibinadamu, Marta Ruedas na Mwakilishi wa UNICEF nchini Sudan, Geert Cappalaere, wamesema Umoja wa Mataifa unadhamiria kuunga mkono kila hatua ya utekelezaji wa mkakati huo.