Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban akutana na Mfalme Abdullah II wa Jordan, asifu usaidizi kwa Wasyria

Ban akutana na Mfalme Abdullah II wa Jordan, asifu usaidizi kwa Wasyria

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amekutana leo na kufanya mazungumzo na Mfalme Abdullah II ibn AL-HUSSEIN wa Jordan, akiwa ameandamana na Rais wa Benki ya Dunia, Jim Yong Kim.

Katibu Mkuu ameeleza shukran zake kwa Jordan kwa kuwapa hifadhi wakimbizi zaidi ya 600,000 wa Syria, na kupongeza kuongezwa kwa usaidizi wa jamii ya kimataifa kwa nchi zilizoathiriwa zaidi na mzozo wa Syria, kama ilivyodhihirika kwenye kongamano la London mwezi Februari.

Ban ameelezea matumaini yake kuwa mkakati mpya wa pamoja baina ya Umoja wa Mataifa na Benki ya Dunia utazalisha usaidizi zaidi kwa Jordan, ili iweze kubadilisha changamoto inazokumbana nazo sasa kuwa fursa.

Aidha, Katibu Mkuu na Mfalme Abdullah II wamejadili kuhusu mchakato wa amani wa Mashariki ya Kati, wakisisitiza umuhimu wa kurejelea mashauriano ya suluhu la mataifa mawili.

Akiwa Jordan pia, Katibu Mkuu amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Jordan, Abdullah Ensour.