Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maridhiano Iraq ni silaha dhidi ya ISIL

Maridhiano Iraq ni silaha dhidi ya ISIL

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amewataka viongozi nchini Iraq kufanyia kazi suala la maridhiano ya kitaifa kwa kuwa ni silaha dhidi ya kundi la kigaidi ISIL ambalo pia hufahamika kama Daesh.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Baghdad jumamosi baada ya mkutano na waziri mkuu Haider al-Abadi na maafisa wengine wakuu wa serikali.

Ban alitembelea Iraq akiambatana na Rais wa benki ya dunia Jim Yong Kim, Rais wa benki ya maendeleo ya Waislamu Dk Ahmad Mohamed Ali Al-Madani. Viongozi hao wako katika ukanda huo siku chache kabla ya mkutano ngazi ya juu kuhusu wakimbizi wa Syria utakaofanyika jumatano mjini Gnevea Uswisi.

Katibu Mkuu amesema maridhiano ni sehemu muhimu ya mkakati wa ushindi dhidi ya ISIL ambayo inashikilia maeneo mengi nchini Iraq na Syria.

Ban amesemaviongozi wengi wa Iraq wanapaswa kufanyakazi pamoja kwa ajili ya amani jumuishi na mafanikio ambapo pia ametaja changamoto zinazoikabili nchi kuwa ni mahitaji ya kibinadamu kutokana na machafuko yaliyosababisha watu milioni 10 kukosa makazi ndani ya nchi.