Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Benki ya Dunia yatangaza ufadhili wa dola milioni 100 kwa shule za Lebanon

Benki ya Dunia yatangaza ufadhili wa dola milioni 100 kwa shule za Lebanon

Rais wa Benki ya Dunia, Jim Yong Kim, ametangaza leo mkakati mpya wa dola milioni 100, unaolenga kuunga mkono mpango wa serikali ya Lebanon wa kuboresha viwango vya elimu na kuwawezesha watoto wote wa Lebanon na watoto wakimbizi wa Syria kwenda shule kufikia mwishoni mwa mwaka wa shule 2016-17.

Ufadhili huo mpya umewezeshwa na uamuzi usio wa kawaida wa Bodi ya Benki ya Dunia kutoa misingi ya ufadhili iliyotengewa nchi za kipato cha chini pekee, na umefanywa wakati Rais wa Benki ya Dunia akiwa ziarani na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Lebanon.

Katika makubaliano hayo, ambayo ni sehemu ya Benki ya Dunia kuzisaidia Lebanon na Jordan kufuatia ukarimu wao kwa kuwapa hifadhi wakimbizi wa Syria, fedha hizo zitasaidia kuboresha viwango vya mfumo wa elimu wa Lebanon ambao sasa unakabiliwa na shinikizo kubwa, pamoja na kusaidia katika kupanua upatikanaji wa elimu kwa watoto wote wa Syria wenye umri kati ya miaka mitatu na 18.

Idadi ya wanafunzi katika shule za Lebanon imeongezeka kwa mamia ya maelfu ya watoto wa Syria, tangu kuzuka kwa vita katika nchi hiyo jirani ya Syria miaka mitano iliyopita.