Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanaowateka wafanyakazi wa UM wakabiliwe kisheria- Ban

Wanaowateka wafanyakazi wa UM wakabiliwe kisheria- Ban

Katibu Mkuu wa umoja huo, Ban Ki-moon, ametoa wito juhudi zaidi zifanywe ili kuwafikisha wanaotenda uhalifu wa kuwateka nyara au kuwatowesha wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa mbele ya sheria na kukomesha ukwepaji sheria.

Ban amesema hayo leo katika ujumbe uliotolewa na msemaji wake katika kuadhimisha siku hii ya mshikamano na wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa waliotekwa na waliotoweka.

Akitaja mfano wa Amer al-Kaissy ambaye alithibishwa kuuawa nchini Iraq mwezi uliopita, baada ya miezi tisa tangu alipotekwa nyara, Ban amerejelea kulaani mauaji hayo na kutoa wito kwa mamlaka za Iraq ziwakabili walioyafanya kisheria.

Mwaka uliopita, wafanyakazi sita wa Umoja wa Mataifa walitekwa na vikundi visivyo vya kiserikali kabla ya kuachiwa huru, huku ishirini wengine wa kiraia wakiwa bado vizuizini hadi sasa. Watano wanashikiliwa na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, na hakuna sababu zilizotolewa kuhusu kukamatwa kwao.