Zeid atiwa wasiwasi na makubaliano ya EU na Uturuki

Zeid atiwa wasiwasi na makubaliano ya EU na Uturuki

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu, Zeid Ra’ad Al Hussein, ameeleza kutiwa wasiwasi mkubwa na makubaliano ya hivi karibuni kati ya Muungano wa Ulaya, EU na Uturuki, akisema makubaliano hayo yanaenda kinyume na kiini chake, na kuzua hofu kuhusu uzuiliaji holela wa wakimbizi na wahamiaji.

Katika taarifa, Zeid amesema lengo la kuwarejesha wakimbizi wote na wahamiaji linakwenda kinyume na hakikisho la kufanya tathmini ya mahitaji binafsi ya kila mmoja wa wakimbizi hao.

Amesema iwapo hakikisho hilo ni la kuaminiwa, basi tathmini ya kila mtu inapaswa kuwezesha watu hao kutorejeshwa kamwe, la sivyo, itaonekana kama uondoaji wa jumla wa wakimbizi na wahamiaji.

Makubaliano ya EU na Uturuki yanataka kesi zote zichunguzwe chini ya agizo la EU kuhusu waomba hifadhi, linalosema kuwa wahamiaji wanaoomba hifadhi au wale ambao maombi yao hayatakubaliwa kulingana na agizo hilo, watarejeshwa Uturuki.