Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lakaribisha tangazo la kusitisha uhasama Yemen

Baraza la Usalama lakaribisha tangazo la kusitisha uhasama Yemen

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, wamekaribisha tangazo la Jumatano Machi 23 2016, lililofanywa na Mjumbe maalum wa Katibu Mkuu kuhusu Yemen, Ismail Ould Cheikh Ahmed, la usitishaji uhasama kote nchini, ambao umepangwa kuanza usiku wa manane Aprili 10, na mazungumzo ya amani yaliyopangwa kuanza Aprili 18, 2016, nchini Kuwait.

Wajumbe hao wa Baraza la Usalama wamekaribisha dhamira ya pande zote husika kushiriki usitishaji uhasama na mazungumzo ya amani.

Aidha, wametoa wito kwa pande hizo kinzani kupunguza ghasia mara moja, na kujiepusha na vitendo vyovyote vinavyoweza kuongeza utata, ili kufungua njia ya kusitisha uhasama.

Wajumbe hao pia wametoa wito kwa pande zote pia kushiriki mazungumzo ya kisiasa kwa njia ya kulegeza misimamo na kujenga, kulingana na maazimio husika ya Baraza la Usalama, hususan azimio namba 2216 la mwaka 2015, bila masharti.