Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchi ziungane kutokomeza TB- WHO

Nchi ziungane kutokomeza TB- WHO

Mamilioni ya maisha ya watu yameokolewa kutoka ugonjwa wa kifua kikuu tangu mwaka 2000, lakini vita vya kutokomeza ugonjwa huo vimefaulu kwa nusu tu wamesema wataalamu wa afya wa Umoja wa mataifa leo, ikiwa ni siku ya kimataifa ya kifua kikuu inayoadhimishwa kila mwaka Machi 24.

Kwa mujibu wa shirika la afya duniani WHO watu zaidi ya milioni 9 huugua kikua kikuu au TB kila mwaka na milioni 1.5 kati yao hufariki dunia kwa maradhi hayo.

Na sasa katika wito wa kutokomeza kabisa ugonjwa huo WHO inazitaka nchi kuongeza kasi ya juhudi zao na kutumia vyema nyenzo mpya za uchunguzi na madawa. Kifua kikuu kinaongoza kwa kuua katika maradhi ya kuambukiza kuliko hata HIV na ukimwi.

Ingawa kasi ya maambukizi imepungua kwa nusu lakini WHO inaonya kwamba vita bado haijafaulu na kutoa wito kwa nchi na wadau wengine kushirikiana kutokomeza ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030 kama ajenda muhimu ya maendeleo endelevu. Dokta Mario Raviglione, mkurugenzi wa WHO kuhusu mpango wa kimataifa wa kifua kikuu anafunguka

(SAUTI YA DR RAVIGLIONE)

“Sote tunajua udhaifu wa vifaa tulivyonavyo leo hii, sio kwamba havitibu watu, vinatibu watu , lakini tungeweza kufanya vitu kwa ufanisi Zaidi kama tungekuwa na ufadhili Zaidi katika utafiti. Tunahitaji ushirikiano mkubwa na serikali, ndani ya serikali, baina ya serikali, na sekta binafsi na mashirika ya maendeleo. Ina ni mtazamo wa jamii nzima”

Zaidi ya asilimia 95 ya vifo vya TB hutokea katika nchi za kipato cha chini na wastan ambako vita dhidi ya maradhi hayo inaweza kuwa changamoto kubwa.