Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

MONUSCO yalaani mauaji ya mwanaharakati wa haki Kivu Kusini

MONUSCO yalaani mauaji ya mwanaharakati wa haki Kivu Kusini

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, Maman Sidikou amelaani vikali mauaji ya mwanaharakati wa haki za binadamu yaliyotokea kwenye eneo la Kavumu, Kivu Kusini nchini humo.

Taarifa iliyotolewa kwa pamoja na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa DRC MONUSCO na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu nchini humo imeeleza kwamba mwanaharakati huyo ambaye alikuwa mratibu wa shirika lisilo la kiserikali la Organisation populaire pour la paix anadaiwa kuuawa na watu wenye silaha ambao walivamia nyumba yake akiwemo na na mke na watoto wake na kumpiga risasi tatu kifuani.

MONUSCO imeongeza kwamba mwanaharakati huyo alifahamika kwa kushughulikia masuala ya utekaji nyara na ubakaji kwenye eneo la Kavumu na kumulika udhaifu wa mamlaka za serikali katika kubaliana na masuala hayo.

Bwana Sidikou amekaribisha kufunguliwa kwa uchunguzi na mwendesha mashataka wa kijeshi akiongeza kwamba ni lazima haki itendeke.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Ofisi ya haki za binadamu nchini DRC Jose Maria Aranaz amesisitiza umuhimu wa kuunda haraka mfumo wa kulinda wanaharakati wa haki nchini humo.