Misri acha kukandamiza mashirika ya kiraia- Zeid

23 Machi 2016

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu katika Umoja wa Mataifa Zeid Ra’ad Al Hussein ametaka serikali ya Misri iache kukandamiza mashirika ya kiraia.

Zeid ametoa wito huo leo kufuatia habari za kufungwa kwa mamia ya mashirika ya kiraia nchini humo sanjari na kufunguliwa mashtaka kwa watetezi wa haki za  binadamu kwa kazi yao halali tangu mwezi Novemba mwaka 2014.

Amesema kinachofanyika kinaonekana kama msako dhidi ya vikundi fulani vya kiraia nchini Misri na hiyo lazima ikome.

Zeid ametolea mfano hukumu inayotarajiwa kutolewa kesho na mahakama nchini Misri dhidi ya watetezi wawili wa haki za binadamu ikilenga kuzuia mali zao kwa tuhuma za kupokea dola Milioni Moja na Nusu kutoka serikali ya kigeni.

Kamishna Zeid amesema kila mtu ana haki ya kupokea fedha kuendeleza haki za binadamu kwa njia ya amani na hivyo serikali ya Misri iache mara moja mashtaka yote dhidi ya watetezi wa haki wakiwemo wawili hao Hossam Bahgat and Gamal Eid.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter