Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nyota wa muziki toka Mali atajwa kuwa balozi mwema wa UNHCR

Nyota wa muziki toka Mali atajwa kuwa balozi mwema wa UNHCR

Mtunzi na mwimbaji nyota wa muziki kutoka nchini Mali Rokia Traoré ametangwaza na shirika la Umoja wa mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR kuwa balozi wake mwema wa kanda ya Afrika Magharibi na Kati.

Baada ya kupokea uteuzi rasmi Bi Traoré, amesema ni heshima kubwa kuchukua jukumu hilo hasa wakati huu muhimu kwa wakimbizi.

Nyota huyo aliyezaliwa Bamako mjini kuu wa Mali , na mshindi wa tuzo ya muziki amekuwa akifanya kazi na UNHCR tangu mwaka 2013 katika kuelimisha kuhusu wanaolazimishwa kukimbia makazi yao hasa barani Afrika.

Mwanamuziki huyo ameshawatembelea wakimbizi wa Mali nchini Burkina Faso, kutumbuiza katika hafla ya tuzo ya wakimbizi ya Nansen mjini Geneva mwaka 2014 na kuunga mkono kampeni ya UNHCR ya Ibelong ya kutokomeza kutokuwa na utaifa ya mwaka 2014.

Katika kuadhimisha uteuzi wake kama balozi mwema , Traoré ametoa wimbo maalumu katika albam ya video yake mpya iitwayo "Né So," ikimaanisha “Nyumbani” katika lugha yake ya kibambara. Video hiyo ni maalumu kwa ajili ya wakimbizi wa Mali pamoja na wote waliolazimika kukimbia makwao kote duniani.