Skip to main content

Watoto milioni 87 wa chini ya miaka 7 hawana wakijuacho zaidi ya vita:UNICEF

Watoto milioni 87 wa chini ya miaka 7 hawana wakijuacho zaidi ya vita:UNICEF

Zaidi ya watoto milioni 86.7 wa chini ya umri wa miaka 7 wameishi maisha yao yote katika maeneo ya vita na kuweka maendeleo ya ubongo wao hatarini limesema leo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF.

Katika miaka saba ya mwanzo wa maisha ya mtoto ubongo wake una uwezo wa kuamsha seli 1,000 za ubongo kila sekunde. Kila moja ya seli hizo ziitwazo neva zinauwezo wa kuungana na neva zingine 10,000 kwa sekunde. Na ubongo ndio muhimili wa mustakhbali wa mtoto katika kutanabahi afya zao, jinsi wanavyohisi na uwezo wa kujifunza.

Kwa mujibu wa UNICEF watoto wanaoishi kwenye vita mara nyingi wanashuhudia ukatili uliokithiri, na hivyo kuwaweka katika hatari ya maisha yaliyoghubikwa na msongo wa mawazo, hali ambayo huzuia uhusiano muhimu wa neva katika ubongo na kuleta madhara makubwa ya maisha kwa maendeleo yao ya utambuzi, kijamii na kimwili.

Mbali ya athari hizo za kimwili UNICEF inasema pia wana hatari ya kuathirika kihisia.

Takwimu zinaonyesha kwamba mtoto mmoja kati ya 11 wenye umri wa miaka sita au chini ya hapo wametumia muda muhimu wa maendeleo ya ubongo wao katika vita.