Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Imani za kishirikina zachochea mauaji ya Albino:Ripoti

Imani za kishirikina zachochea mauaji ya Albino:Ripoti

Watu wenye ulemavu wa ngozi au Albino wamekuwa wakisakwa kwa ajili ya masuala ya kishirikina , viungo vyao kikikatwa kwa mapanga na hata makaburi yao kufukuliwa , ameonya mtaalamu wa Umoja wa Mataifa Ikponwosa Ero katika ripoti yake ya kwanza kwenye baraza la haki za binadamu. Taarifa kamili na Priscilla Lecomte.

(Taarifa ya Priscilla)

Tangu Bi, Ero kuanza kazi yake miezi minane iliyopita kama mtaalamu huru kwa ajili ya kufurahia haki za binadamu kwa ajili ya watu wenye ulemavu wa ngozi , kumekuwa na taariza za mashambulizi 40 katika nchi saba , lakini amesema hayo yanawakilisha sehemu ndogo tuu kwani mashambulizi mengi yanafanyika kwa siri hasa vijijini na hayaripotiwi na mengine yanajumuisha hata ndugu wa familia wa waathirika.

Amesema “Imani potofu na hatari ni chanzo cha mashambulizi haya dhidi ya watu wasio na hatia, wengi wanaamini watu wenye ulemavu wa ngozi sio binadamu bali ni mizimu na hawawezi kufa bali kutoweka, cha kusikitisha Zaidi wengi wanaamini hali hiyo ya ulemavu wa ngozi ni laana.”

Katika ripoti yake ameainisha mipango ya kubaini chanzo cha mashambulizi hayo ambayo inajumuisha kuelewa , kuelezea na kutambua vitendo vya kishirikina, jinsi vinavyofanyika na athari zake kwa watu wenye ulemavu wa ngozi.

Ameendelea kusema kukomesha mashambulizi kutahijaji kufanyika uchunguzi wa haraka wa madai yote na kuwachukulia hatua wahusika ikiwa ni pamoja na hatua za kusitisha usafirishaji haramu wa viungo vyao. Katika baadhi ya maeneo mtu 1 kati ya 70 ana ulemavu wa ngozi japo kwa ujumla ni mtu 1 kati ya 5000 au 1 kati ya 20,000 ndio wana ulemavu huo duniani kote. Kwa mujibu wa taarifa kiungo cha albino mkono au mguu huuzwa kwa takribani dola 2000 na maiti nzima huuzwa dola 75,000.