Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mabadiliko ya tabianchi mwiba kwa maji safi na salama- UNICEF

Mabadiliko ya tabianchi mwiba kwa maji safi na salama- UNICEF

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF limesema mabadiliko ya tabianchi yanatishia upatikanaji wa maji safi na salama kwa mamilioni ya watoto wanaoishi kwenye maeneo yanayokumbwa na ukame au mafuriko.

Mkuu wa Mradi wa Maji Safi na Huduma za Kujisafi wa UNICEF Sanjay Wijeserkera amesema katika taarifa kuwa ajenda 2030 inataka huduma ya maji kwa wote ambayo ni changamoto ya aina yake kuliko hata wakati wa malengo ya milenia.

Mathalani amesema upatikanaji ni hatua moja lakini usalama wake ni changamoto kwani wakati wa ukame watu wanakimbilia maji yasiyo salama na mafuriko nayo huharibu miundombinu ya maji hata kuchanganyika kwa mabomba ya maji safi na yale ya majitaka.

Amesema watoto karibu Milioni 160 wenye umri wa chini ya miaka mitano wako hatarini zaidi wengi wao wakiwa nchi za Afrika Kusini mwa jangwa la Sahara pamoja na Asia.

Kwa mantiki hiyo kuanzia tarehe 22 mwezi ujao, UNICEF itazindua kampeni kupitia mtandao wa kijamii wa Instagram kuelimisha umma juu ya uhusiano kati ya maji, mazingira na mabadiliko ya tabianchi wakitumia #ClimateChain