Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali Palestina si endelevu, asema mtaalam wa haki wa UM

Hali Palestina si endelevu, asema mtaalam wa haki wa UM

Mtaalam maalum kuhusu maeneo ya Palestina yaliyokaliwa, Makarim Wibisono, ameonya kuwa hali katika maeneo ya Palestina yalokaliwa inazidi kuwa tete huku raia wakishinikizwa kufanya vitendo vinavyoonyesha kukata tamaa na vikosi vya Israel vikitumia nguvu kupindukia.

Bwana Wibisono amesema hayo leo Jumatatu mbele ya Baraza la Haki za Binadamu, katika kikao ambacho kimesusiwa na ujumbe wa Israel.

Amelaani vitendo vya ghasia, akiongeza kuwa amani haiwezi kupatikana bila uwajibikaji.

Akimulika hali ya hivi karibuni, ambapo machafuko yaliongezeka Ukingo wa Magharibi, Wibisono amesema hali ya taharuki imetanda.

“Wakati kuchanganyikiwa kukiongezeka kutokana na kukaliwa kwa miongo mingi, pande zote zinachukua hatua za kukata tamaa zaidi, na hivyo kuwatia raia hatarini.”

Amesema mamia ya waPalestina wamo vizuizini, huku kupanua kwa makazi ya waIsraeli Ukingo wa Magharibi kukichangia ukiukwaji wa haki za Wapalestina mara kwa mara.