Skip to main content

Ntaganzwa ahamishiwa Rwanda kujibu mashtaka ya mauaji ya halaiki 1994

Ntaganzwa ahamishiwa Rwanda kujibu mashtaka ya mauaji ya halaiki 1994

Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC imempeleka Rwanda mmoja wa watoro tisa wanaosakwa kujibu mashtaka dhidi ya mauaji ya halaiki nchini humo mwaka 1994.

Mtoro huyo Ladislas Ntaganzwa, ambaye ni meya wa zamani wa eneo la Nyakizu anakabiliwa na mashtaka ya mauaji ya halaiki na uhalifu dhidi ya binadamu ikwiemo ubakaji, wakati wa mauaji ya maelfu ya watutsi kwenye maeneo kadhaa ikiwamo parokia ya Cyahinda na huko Gasasa ambapo pia wahutu wenye msimamo wa kadri waliuawa.

Uhamisho wake ni kwa mujibu wa hati ya kukamatwa iliyotolewa na mfumo uliorithi mahakama ya kimataifa ya uhalifu kwa Rwanda, MICT ambapo mwendesha mashtaka wake Serge Barammertz amepongeza hatua ya DRC.

Watoro wengine Nane bado hawajulikani waliko wakiwemo Felicien Kabuga, Augustin Bizimana na Protais Mpiranya ambapo MICT imeomba jamii ya kimataifa kuwezesha kukamatwa kwao.