Skip to main content

Matumizi bora ya nishati kuipatia Kenya dola Milioni 188 kila mwaka- UNEP

Matumizi bora ya nishati kuipatia Kenya dola Milioni 188 kila mwaka- UNEP

Kuongezeka kwa matumizi endelevu  ya misitu nchini Kenya kunaweza kupunguza kwa asilimia 27 utoaji wa hewa ya ukaa na wakati huo huo nchi hiyo kujipatia dola Milioni 188 kwa mwaka.

Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti ya pamoja ya serikali ya Kenya na shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa UNEP iliyotolewa leo ikiwa ni siku ya misitu duniani.

Mathalani imesema kuwekeza katika mbinu bora za kuchakata mazao ya misitu kunaweza kupunguza ukataji hovyo wa miti na uharibifu wa misitu na hivyo kupunguza kwa tani Milioni 20 kiwango cha hewa ya ukaa kwa mwaka kitokanacho na matumizi hovyo ya ardhi na kilimo.

Ripoti imesema gharama za uwekezaji kama vile matumizi ya nishati endelevu majumbani halikadhalika nishati salama kwenye viwanda kutagharimu dola Milioni 39 ambayo ni pungufu kwa asilimia 25 ya mapato yanayotarajiwa.

Akizungumzia ripoti hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP Achim Steiner amesema mapendekezo hayo yanadhihirisha ni kwa jinsi gani sekta ya misitu inaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa ahadi za Kenya katika mkataba wa mabadiliko ya tabianchi ikiwemo nishati salama na kupunguza matumizi ya kuni.