Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bado safari ni ndefu kutokomeza ubaguzi wa rangi: Ban

Bado safari ni ndefu kutokomeza ubaguzi wa rangi: Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa MAtiafa Ban Ki-moon ameelezea wasiwasi mkubwa kuhusu ongezeko la ubaguzi na ghasia inayohusiana na chuki za kibaguzi duniani kote.

Maoni hayo ameyatoa akihutubia kikao maalum cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kilichofanyika leo kwa ajili siku ya kutokomeza ubaguzi wa rangi, ambayo itaadhimishwa tarehe 21 Machi.

Bwana Ban ameaanza kwa kupongeza hatua zilizofikiwa katika kuhakikisha usawa wa haki na kutokomeza ubaguzi, tangu mauaji ya waandamanaji dhidi ya ubaguzi wa rangi, mjini Sharpeville, Afrika Kusini, tarehe 21, Machi, mwaka 1960.

Hata hivyo amesema mzozo na mivutano dhidi ya vikundi vya watu walio wachache imeongezeka, akimulika hasa ghasia, chuki na mashambulizi dhidi ya wahamiaji, wakimbizi na waislamu.

(Sauti ya Bwana Ban)

“Vyama vya kisiasa venye itikadi kali vinachochea mgawanyiko wa jamii na kuongeza hatari, na sauti zilizokuwa na busara zamani sasa zinachochea hofu, ikikumbusha nyakati mbaya za historia ya karne iliyopita. Hayo yote yanaongeza hatari ya kuvunjwa kwa mshikamano wa jamii, ukosefu wa utulivu na mizozo.”

Katibu Mkuu amesisitiza kwamba mashambulizi dhidi ya kundi moja ni sawa na mashambulizi dhidi ya wote, akisema ni lazima kudumisha haki na utu kwa wote.