Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Furaha ni zaidi ya pesa, ni kuridhika na kujali wengine

Furaha ni zaidi ya pesa, ni kuridhika na kujali wengine

Ikiwa leo ni siku ya furaha duniani, ujumbe ukiwa furaha na ustawi wa binadamu na sayari ya dunia kwa maendeleo endelevu, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ametaka kila mtu, serikali na taasisi kusongesha kampeni hiyo ya kuwa na sayari bora.

Katika ujumbe wake, Ban amesema zama za sasa zikigubikwa na ukosefu wa haki, ni vyema kutumia siku ya leo kutambua kuwa amani, ustawi wa binadamu na furaha vinapaswa kupatiwa kipaumbele.

Amesema ni wakati wa kutambua umuhimu wa mtu kuridhika na kubaini kuwa kila mmoja anawajibika na utu wa kila mtu.

Akizungumza awali na waandishi wa habari mjini New York, Marekani kuhusu siku ya furaha duniani, Naibu Mwakilishi wa kudumu wa Sao Tome na Principe kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Angelo Toriello amesema furaha si kitu cha anasa bali ni jambo muhimu kwa kila mtu kwenye jamii na amepongeza nchi zlizochukua hatua kama vile Bhutan kuweka vigezo vya kupima furaha na kwamba.

(Sauti ya Balozi Toriello)

“Tunaweza kushiriki kwa dhati kutatua matatizo tunapokuwa na furaha zaidi, na siyo tunapokuwa na msongo. Msongo hauwezi kupatia suluhu matatizo, bali unaleta matatizo. Kwa hiyo kwa nini tusiwe na furaha?”

image
Katibu Mkuu wa UM Ban Ki-moon katika picha ya pamoja na vikaragosi vya Angry birds kwenye Umoja wa Mataifa. (Picha: UN/Dianne Penn)
Naye Dkt. Judy Kuriansky mshauri na mhadhiri kuhusu masuala ya saikolojia akizungumza kwenye mkutano  huo amesema..

(Sauti ya Dkt Judy)

“Serikali katika jengo hili sasa zinakubali kuwa si pesa pekee zinazofanya watu wawe na furaha. Tunapaswa sasa kwenda mbali zaidi ya pato la ndani la taifa na kuangalia watu wanajisikia vipi kuhusu ustawi wao.”

Katika kuadhimisha siku ya furaha duniani, Umoja wa Mataifa unatumia vikaragosi vya Angrybird kuchagiza umuhimu wa kulinda sayari ya dunia kwa furaha ya kila mkazi. #AngryBirdsHappyPlanet