Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Qatar: UM wakaribisha kuachiliwa mshairi al-Ajami, lakini watoa wito wa kutathinini mfumo wa sheria nchini humo

Qatar: UM wakaribisha kuachiliwa mshairi al-Ajami, lakini watoa wito wa kutathinini mfumo wa sheria nchini humo

Wataalamu watatu wa haki za binadamu wa Umoja wa mataifa, leo wamekaribisha kuachiliwa kwa mshairi wa Qatar Mohammed al-Ajami huku wakiitaka serikali ya Qatar kufikiria kutathinmini  sheria na mfumo wake wa haki ambao ulisababisha kufungwa kwa mshairi huyo.

Bwana al-Ajami alipewa msamaha wa Emiri  Machi 15 na kuachiliwa kutoka jela ambako alikuwa akitumikia kifungo cha miaka 15 kwa kuandika na kughani shairi linalodaiwa kumkosoa mwana mfalme wa Qatar, kusifia mapinduzi ya Tunisia na kushutumu ufisadi na ukandamizaji wa watawala wa Kiarabu.

Mwakilishi maalumu wa wa Umoja wa mataifa kuhusu haki za utamaduni Karima Bennoune, mwakilishi kuhusu uhuru wa kujieleza David Kaye na mwakilishi kuhusu uhuru wa mahakama  Mónica Pinto wamesema wanashukuru kwamba Bwana al-Ajami ameachiliwa na kuweza kuungana na familia yake, lakini msamaha huo hautanabaishi kufungwa kwakwe kimakosa na hakuna hakikisho kwamba haki na uhuru wa raia utaheshimiwa baadaye.

Wataalamu hao wamesisitiza kwamba sheria za Qatar na sera za serikali ni lazima ziwalinde wale wanaotekeleza haki zao za uhuru wa kujieleza, ikiwemo kujieleza kupitia utamaduni, na haki zao za kushiriki masuala ya utamaduni badala ya kuwahukumu.