Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Msafara mwingine wafikia watu waliozingirwa Syria, msaada zaidi wahitajika- OCHA

Msafara mwingine wafikia watu waliozingirwa Syria, msaada zaidi wahitajika- OCHA

Nchini Syria, misafara ya pamoja ya mashirika ya kibinadamu imefanikiwa kufikia miji ya Madaya, Zabadani, Foah na Kafraya ambayo hadi sasa imezingiriwa na pande kinzani za mzozo.

Taarifa ya Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu (OCHA) imeeleza kwamba watu 60,000 wamepatiwa misaada ya chakula, vifaa tiba, maji safi na salama na vifaa vingine mbali mbali.

Hadi sasa, ni watu 260,000 ambao wamefikiwa na misafara ya kibinadamu tangu mwanzo wa mwaka huu wa 2016.

Hata hivyo  OCHA imesisitiza kwamba msaada zaidi unahitajika ili kusaidia watu wote milioni 4.6 wanaoishi kwenye maeneo yanayofikika kwa taabu na yanayozingirwa nchini Syria.